Hamia kwako na Watumishi Housing Company, Tanzania

Polisi Tanzania yanasa mtandao wa kimataifa wa majambazi

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limefanikiwa kuwakamata zaidi ya majambazi 10 wanaotuhumiwa kuhusika na matukio mbalimbali ya ujambazi jijini Dar es Salaam, ikiwemo uporaji wa fedha katika benki na mauaji ya Polisi.
Akitangaza kufanikiwa kwa operesheni maalumu ya kuwasaka majambazi kwenye mkoa wa Dar es Salaam, kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, amesema baada ya kuendesha msako mahsusi kwenye maeneo kadhaa ya jiji, wamefanikiwa kuwakamata majambazi zaidi ya kumi pamoja na silaha zaidi ya 22 na rsasi zake.

Operesheni hii ya jeshi la Polisi nchini Tanzania, ilianzishwa siku kadhaa baada ya tukio la kuuawa kwa askari watatu kwenye eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam, ambapo majambazi wenye silaha waliwavamia Polisi waliokuwa wakibadilishana lindo kwenye moja ya benki.

Sirro amesema kuwa majambazi watatu kati ya 10 ambao wanashikiliwa, wamekiri kuhusika kwenye matukio mbalimbali, ikiwemo ya uporaji katika benki mbili mwaka 2014, uvamizi wa kituo cha Polisi Stakishari na kuua Polisi wanne na kutoweka na silaha za SMG.

Kamanda Sirro ameongeza kuwa, baada ya kuwahoji watuhumiwa hao watatu na kukiri kuhusika kwenye matukio ya kihalifu, walikubali kuwapeleka Polisi kwenye eneo ambako wamekodisha nyumba wanayoitumia kupanga vitendo vya kihalifu.

Kuhusu operesheni iliyofanyika kwenye misitu ya eneo la mji wa Vikindu, kamanda Sirro, amesema Polisi waliweka mtego kwa kuwatumia sehemu ya majambazi waliowakamata, ambapo waliwatanguliza kwenye eneo hilo kabla ya wao wenyewe kwa wenyewe kuanza kukabiliana baada ya kuona wamewasili na Polisi.
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limeongeza kuwa mtandao huu wa majambazo ni wa kimataifa kwa kile linachosema, waliokamatwa wamekiri kushirikiana na raia wa kigeni kutoka nchini Kenya, ambao jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka.

Polisi inasema silaha zilizokamatwa, zimo silaha kadhaa za kijeshi ambazo hutumiwa kwenye vita, ambapo pia zaidi ya risasi 800 zilikamatwa kwenye operesheni hiyo ya jeshi la Polisi.
Miongoni mwa vitu vingine vilivyokamatwa kwenye operesheni hiyo ni pamoja na magari yanayodaiwa kuwa yalikuwa yakitumika kwenye wizi, mitambo ya kuvunjia milango, mapanga na mitambo ya CCTV.
Share on Google Plus

About Ngoma Kali Tz

0 comments:

Post a Comment