Hamia kwako na Watumishi Housing Company, Tanzania

Msiba wa Mzee Samwel Sitta zimemfikia na Rais Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai kufuatia kifo cha Spika Mstaafu na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo Tabora Samwel Sitta.
Mzee Samwel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Technical University of Munich Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu tangu mwezi uliopita.
sitta-jpm
Rais Magufuli alipokwenda kumjulia hali Mzee Sitta nyumbani Dar es salaam baada ya kupata taarifa za kuugua kwake.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Samwel Sitta na Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.
“Nitamkumbuka Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za siasa na Serikali.
“Kupitia kwako Mhe. Spika naomba kutoa pole nyingi kwa Mke wa Marehemu Mhe. Magreth Sitta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Urambo na familia nzima ya marehemu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi wa Urambo Mkoani Tabora na watu wote walioguswa na msiba huu” amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.
Dkt. Magufuli amesema anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na amewaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi, Ameni”
Taarifa imetolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU. Dar es Salaam
07 Novemba, 2016
Share on Google Plus

About Ngoma Kali Tz

0 comments:

Post a Comment