Hamia kwako na Watumishi Housing Company, Tanzania

Matteo Renzi ajiuzulu baada ya kushindwa kura ya maamuzi Italia


Matteo Renzi, akiongea Palazzo Chigi mjini Roma, Italia, 4 Desemba 2016Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi amejiuzulu baada ya kukubali kushindwa katika kura ya maamuzi kuhusu marekebisho ya katiba nchini humo.Akihutubia wanahabari usiku, kiongozi huyo alisema anakubali lawama kutokana na matokeo hayo, na kwamba kambi ya La, ambayo ilipinga mageuzi hayo, sasa inafaa kutoa mapendekezo ya mwelekeo kutoka sasa.
Baada ya sehemu kubwa ya kura kuhesabiwa, kambi ya La inaongoza kwa 60% dhidi ya 40% za Ndio.
Waliojitokeza kupiga kura walikuwa takriban 70% ya wapiga kura wote waliojiandikisha, jambo linalotazamwa na wengi kama ishara yao kuonesha kutoridhishwa kwao na waziri mkuu huyo.
"Kila la heri kwetu sote," Bw Renzi aliwaambia wanahabari.

Alieleza kuwa ataitisha mkutano wa baraza la mawaziri baadaye adhuhuri Jumatatu.
Baadaye, atawasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa rais wa Italia, baada ya kuhudumu kwa miaka miwili unusu.
Bw Renzi alisema mageuzi aliyokuwa amependekeza yangeunguza urasimu mwingi nchini Italia na kuifanya kuwa na ushindani zaidi.
Lakini kura hiyo ya maamuzi ilitazamwa na wengi kama fursa ya kueleza kutofurahishwa kwao na waziri mkuu huyo.

Kuraya Hapana iliungwa mkono na vyama vyenye sera za kujipendekeza kwa raia wengi.
Aidha, kura hiyo ya maamuzi ilitazamwa kama kipima joto cha hisia za kupinga mfumo wa kawaida wa utawala barani Ulaya.
Chama cha Five Star Movement, kilichoongoza kampeni hiyo kimesema kinajiandaa kutawala Italia sasa kufuatia kujiuzulu kwa Bw Renzi. Kiongozi wa kundi hilo alikuwa mchekeshaji Beppe Grillo.
"Kuanzia kesho, tutaanza kufanyia kazi serikali ya Five Star," mmoja wa viongozi wake, Luigi Di Maio, alisema.
Kiongozi wa upinzani Matteo Salvini, wa chama cha Northern League kinachowapinga wahamiaji, alitaja kura hiyo ya maamuzi kama "ushindi wa raia dhidi ya nguvu zinazodhibiti robo tatu ya dunia."
Vyama vingine vya mrengo wa kulia barani Ulaya vimefurahia matokeo hayo.
Kiongozi wa chama cha Front National nchini Ufaransa, Marine Le Pen, amekipongeza chama cha Northern League kupitia Twitter.
"Wataliano wamejitenga na EU na Renzi. Lazima tutegee sikio kiu hii ya mataifa kutaka kuwa huru," alisema.
Thamani ya sarafu ya euro ilishuka mara moja baada ya matokeo ya mapema kutangazwa.
Kumekuwepo na wasiwasi kuhusu uthabiti wa Italia kisiasa, taifa ambalo ni la tatu kwa ukubwa kiuchumi katika mataifa yanayotumia sarafu ya euro.

Kura ya La ina maana gani?

Kampeni ya La nchini Italia iliongozwa na kundi lililopinga mfumo wa kawaida wa utawala cha Five Star Movement, lililoongozwa na Beppe Grillo.
Wanataka kufanyike kura ya maamuzi ya kuamua iwapo Italia inafaa kuendelea kutumia sarafu ya euro
Vyama vikuu vilivyopinga kura hiyo, Five Star Movement na Northern League - wanaopinga wahamiaji -, ni vyama vyenye sera za kujipendekeza kwa raia.
Kura hiyo ya maamuzi imefanyika miezi kadha baada ya kura ya Brexit nchini Uingereza ambapo Waingereza waliunga mkono kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya (EU) mwezi Juni.
Aidha, imefanyika huku chama cha kupinga wahamiaji Ufaransa, Front National, na vyama vingine vya kujipendekeza kwa raia vikiendelea kupata umaarufu Ulaya na kwingineko.
Kadhalika, ni chini ya mwezi mmoja baada ya ushindi wa Donald Trump nchini Marekani.
Wataliano takriban 50 milioni walikuwa wamejiandikisha kupiga kura, wengi wao wakiwa wamevunjwa moyo na miaka mingi ya kukwama kwa ukuaji wa uchumi nchini Italia.
Share on Google Plus

About Ngoma Kali Tz

0 comments:

Post a Comment