Hamia kwako na Watumishi Housing Company, Tanzania

TAARIFA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA


unnamed

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.
KUPATIKANA NA DAWA ZA KULEVYA [BHANGI]
Mnamo tarehe 13.06.2017 kuanzia majira saa 17:00 jioni hadi saa 19:00 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Kijiji cha Ipinda kilichopo Kata ya Ihango, Tarafa ya Iyunga, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya.
Katika msako huo, watu wawili walikamatwa wakiwa na Bhangi, ambapo ALLY JOSEPH [67] Mkazi wa kijiji cha Ipinda ambaye alikamatwa akiwa na bhangi kavu debe 01 iliyokuwa imehifadhiwa kwenye mfuko wa Salfeti. Aidha Mtuhumiwa DAUD ALLY [32] Mkazi wa kijiji cha Ipinda ambaye alikamatwa akiwa na Bhangi Kilo 05 na miche 670 ya bhangi ambayo alikuwa ameipanda kwenye shamba la mahindi. Watuhumiwa ni wauzaji na wakulima wa bhangi.
Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya Upelelezi kukamilika.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo kumekuwa na taarifa 02 za vifo kama ifuatavyo:-
Mnamo tarehe 13.06.2017 majira ya saa 18:00 jioni huko Ilembo, Kata ya Nsalala, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya, Mwanafunzi wa Chekechea aliyefahamika kwa jina la MIRIAM MICHAEL [06] Mkazi wa Ilembo alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali Teule ya Ifisi kwa matibabu baada ya kula mboga zinazodhaniwa kuwa na sumu.
Marehemu alifikishwa Hospitalini hapo akiwa na mtoto mwenzake aitwaye FELISTER MUSSA [07] Mkazi wa Ilembo kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Inadaiwa kuwa chanzo cha kifo hicho ni baada ya marehemu na mwenzake kula mboga za majani ya maboga ambazo inadaiwa zilipikwa kwenye chombo ambacho kinasadikiwa kilitunzia sumu ya kuulia wadudu ambayo bado haijajulikana hadi sasa.
Hali ya kupoteza fahamu ilitokea wakati marehemu na mtoto mwenzake wakicheza baada ya kula na kuanza kulegea na mwili kukosa nguvu. FELISTER MUSSA bado amelazwa Hospitali Teule Ifisi akiendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa ndugu kwa mazishi.
Mnamo tarehe 13.06.2017 majira ya saa 18:30 jioni huko Kitongoji cha Itumbi, Kijiji na Kata ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la NDELE HAMIS [27] Mkazi wa Matundasi alifariki dunia akiwa ndani ya shimo alimokuwa akichimba madini aina ya dhahabu.
Aidha katika tukio hilo, watu wengine watatu waliokuwa pamoja na marehemu walijeruhiwa na wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri. Chanzo cha kifo kinasadikiwa ni kukosa hewa baada ya mtambo wa kutoa hewa safi [Oxygen] kupata hitilafu wakati wakiwa ndani ya shimo hilo lenye urefu wa mita 12. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa uchunguzi wa kitabibu.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa jamii kuacha kutumia Dawa za Kulevya kwani ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa afya ya mtumiaji. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za mtu/watu au kikundi cha watu wanaojihusisha na kulima, kuuza/kusambaza dawa za kulevya [bhangi] ili wakamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
                                             Imesainiwa na:
 [DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment