Hamia kwako na Watumishi Housing Company, Tanzania

Hasara soko la Sido Mbeya ni bil 14.2/-

HASARA iliyotokana na ajali ya moto ulioteketeza soko la Sido jijini Mbeya katikati ya mwezi huu ni Sh bilioni 14.2 kwa mujibu wa Tume iliyoundwa kuchunguza ajali hiyo.

Akitoa taarifa ya Tume hiyo kwenye mkutano uliofanyika katika eneo la soko lililoungua, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Hassan Mkwawa alisema baada ya uchunguzi wa siku tano tangu kukabidhiwa majukumu hayo, tume imebaini chanzo cha moto huo ilikuwa shughuli za matumizi ya moto ndani ya soko.

Alisema Tume ilibaini kuwepo na mabaki ya moto yaliyotofautiana na yale ya moto wa mabanda hatua inayodhihirisha kuwa kulikuwepo na moto uliokuwa ukihifadhiwa mara baada ya shughuli za mamalishe kumalizika.

Aliishauri serikali na mamlaka zinazohusika kuchukua tahadhari katika masoko mengine kwa kuweka utaratibu utakaofaa kwenye matumizi ya moto sokoni badala ya kuendelea kuacha shughuli hizo kufanyika kiholela.

Akitoa tamko la serikali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla (pichani) alikubaliana na ushauri wa tume na kutangaza kuwa wafanyabiashara waliounguliwa hawatahamishwa na badala yake watabakia hapo kwa masharti ya kujenga vibanda vya kudumu na kwa kufuata mchoro watakaopewa na wataalamu wa halmashauri.

Makalla aliagiza halmashauri na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) Mkoa wa Mbeya kukutana mara moja na kuingia mkataba wa makubaliano ya kuwaachia wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao kama ilivyoagizwa pia na Rais John Magufuli.

Naye Naibu Spika, Dk Tulia Ackson pamoja na kuwapa pole waathirika wa soko kwa kuwapa jumla ya Sh milioni 10, aliwataka kuendelea kuwa na utulivu huku wakitambua kuwa viongozi wa kiserikali wanatambua mchango wa shughuli zao katika maendeleo ya Taifa.

Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi aliwapongeza wakazi jijini hapa wakiwemo waathirika kwa utulivu waliouonesha wakati wakiendelea kusubiri tamko la serikali. Alivipongeza pia vyombo vya ulinzi na usalama akisema vilionesha ushirikiano mkubwa kuanzia siku ya ajali na wakati taratibu nyingine zikiendelea kufanyika.

Share on Google Plus

About Ngoma Kali Tz

0 comments:

Post a Comment