Hamia kwako na Watumishi Housing Company, Tanzania

WANAVYUO WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZILIZOPO MAUNGONI MWAO


Wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati jijini Mbeya, wamepewa wito kuzitambua na kuzitumia ipasavyo fursa njema zilizopo katika viungo vyao kwani ni njia mahususi ya kuweza kuyafikia malengo yao hasa baada ya kumaliza masomo yao. Wito huo umetolewa na meneja mkuu wa kituo cha redio Dream FM cha jijini humo bwana Grayson Kayombo, katika warsha fupi ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa vyou vinavyoshiriki mashindano ya Dream Inter-College 2017 yaliyoanza kutimua vumbi siku ya jumamosi tarehe 25 Novemba 2017 kwa kushikisha jumla ya vyuo nane katika michezo ya soka na mpira wa pete.


Bwana Kayombo alisisitiza kwamba ni wakati muafaka sasa kwa vijana kutambua fursa nyingi walizonazo kupitia vipaji mbalimbali vilivyomo ndani yao, kwani tunayo mifano dhahiri ya vijana wa ki-Tanzania ambao  wamefanikiwa kiuchumi kwa kuvitumia ipasavyo vipaji walivyonavyo. “Hebu tuwaangalie vijana wenzetu kama vile Mbwana Samata, Hashim Thabeet, Diamond, na wengine wengi  ambao leo wanatuwakilisha vema katika anga za kimataifa kupitia vipaji walivyo navyo. Vijana hawa wanatengeneza pesa nyingi sana kwa kupitia vipaji walivyo nayo. Tena ninyi wanavyuo mna mazingira mazuri ya kufanya vizuri zaidi kwa kuzingatia kwamba mnayo elimu ya kutosha, hivyo mna uwezo mkubwa zaidi wa kupambanua mambo. Wapo vijana wengi wenye vipaji lakini wamefika mahali wamekwama kufika mbali zaidi kwa sababu ya changamotoza kielimu zaidi, hivyo mnapaswa kulitazama hilo pia”, alisema meneja huyo.
Aidha bwana Kayombo aliongeza ufafanuzi kuwa amesema kutumia vyema fursa “njema” zilizomo viungoni mwao kwa kuwa baadhi ya vijana wamekuwa wakivitumia vibaya viungo vyao kwa kufanya matendo hatarishi, yasiyokubalika wala kupendeza mbele ya jamii kwa kuona kuwa ndizo fursa za kujipatia kipato.


“Vipaji tulivyonavyo ni rasilimali kubwa sana ya kutuwezesha kufikia malengo yetu kiuchumi. Lakini hili litawezekana endapo tutakubali kubadili mtazamo wetu na kuachana kung’ang’ania kulalamik na kuimba wimbo wa ukosefu wa ajira. Kama tutachagua kuendeleza fikra za kulalamika basi tuwe tayari kuishia kulalamika kwa muda wote maisha yetu, lakini kama tutachagua kubadili fikra na kuamua kuzitumia ipasavyo fursa tulizonazo, mimi nina hakika tutatoboa kwa ushindi mkubwa sana. Serikali yetu ya awamu ya tano imejikita katika kujenga uchumi wa viwanda, na lazima sisi vijana tuiunge mkono serikali kwa nguvu zote kuujenga uchumi wa viwanda, lakini pia hatuna budi kuitazama sekta ya michezo kama mojawapo ya viwanda vinavyokuwa kwa kasi, na vyenye fursa kubwa ya ajira”, aliongeza bwana Kayombo.
Aidha bwana Kayombo aliwashukuru wadau mbalimbali kwa ushiriki wao katika kufanikisha mashindano hayo kwa njia ya udhamini, ambao ni mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii (SSRA), Airtel, mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSPF Pension Fund, na Ally Rich Sanaa (ARTS) Ltd.


Miongoni mwa vyuo vinavyoshiriki katika mashindano hayo yatakayodumu kwa muda wa wiki mbili hadi tarehe 8 Disemba 2017, ni pamoja na Mzumbe, CBE, TIA, na Tumaini Makumira. Vyou vingine ni MUST, TEKU, Utumishi, na SAUT. Katika hafla hiyo timu shiriki zilipatiwa vifaa vya michezo ikiwa ni pamoja na jezi na mipira kwa michezo yote miwili. Washindi katika mashindano hayo watapatiwa zawadi za vikombe na fedha taslimu.


Mashindano hayo ambayo sasa ni ya mwaka wa pili mfululizo na kujizolea umaarufu mkubwa jijini Mbeya yatahitimishwa kwa tamasha kubwa mnamo tarehe 8 Disemba katika ukumbi wa Mbeya Carnival Lounge litakalowashirikisha wasanii mbalimbali akiwemo Baraka Da Prince, Masoso, D Twice, na wakali wengine kutoka vyuo shiriki.
Share on Google Plus

About Ngoma Kali Tz

0 comments:

Post a Comment